Friday, March 24, 2017

Dkt Abbas: Maafisa Habari Muungeni Mkono Rais Magufuli kwa kutangaza Mafanikio ya SerikaliMkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na Maafisa Habari na Tehama leo Mkoani Morogoro wakati wa mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti za Mikoa  na Halmashauri nchini. Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani yanashirikisha Mikoa ya Arusha, Simiyu, Kilimanjaro, Tanga na Morogoro pamoja na halmashauri zake.
(Na Mpigapicha Wetu)

Na Ismail Ngayonga
Morogoro

SERIKALI imewataka Maafisa Habari na Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya nchini wametakiwa kutangaza mafanikio ya miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongoozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli.

Hayo yamesemwa leo Mjini Morogoro na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa Habari na Maafisa TEHAMA katika mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti za Mikoa na Halmashauri yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).

Kwa mujibu wa Dkt. Abbas alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Mikoa na Halmashauri zake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa zinazowekwa katika tovuti hizo  zinaonyesha mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo.

“Ipo miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ikiwemo miradi ya umeme vijiji, ambapo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa za utekelezaji wa miradi inawafikia wananchi” alisema Dkt. Abbas.

Aliongeza kuwa  lengo la Serikali ya Awamu ya Tano inayooongozwa na Rais Dkt. John  Pombe Magaufuli ni kuleta matokeo ya haraka kwa wananchi wake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha taarifa mbalimbali za mafaniko katika maeneo yao ya kazi zinatangazwa kwa kuzingatia  muda na wakati.

Dkt. Abbas alisema kuwa Serikali ipo mbioni kuanza utaratibu wa kupima utendaji kazi wa Maafisa Habari na Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya ili kuangalia ni kiasi gani wameweza kutangaza mafanikio ya Serikali katika maeneo yao ya kazi.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbas alisema utaratibu huo wa upimaji utaweza kuainisha Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Mikoa na Wilaya  zinatoa na zisizotoa taarifa zake kwa umma, ambapo taarifa hiyo itaweza kuwasilishwa katika Mamlaka za juu Serikalini kwa ajili ya utekelezaji.

Aidha alisema kwa sasa suala la utoaji wa taarifa kwa umma si suala la utashi badala yake ni matakwa ya kisheria, hivyo Serikali inaandaa barua zitazoelezwa kwa Watendaji wakuu katika mamlaka za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kuhusu umuhimu wa utoaji wa taarifa kwa umma.

“Kwa sasa tuna sheria ya huduma za habari na sheria ya haki ya kupata taarifa, ambazo zote zinasisitiza na kutoa maelekezo kwa taasisi zote za umma kutoa taarifa kwa wananchi” alisema Dkt Abbas.

Alisema kuwa ili kutekeleza vyema majukumu yao msingi ni wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kuhakikisha kuwa wanatumia vyema mitandao ya kijamii katika utoaji wa taarifa za Serikali, kwani kwa sasa ulimwengu upo katika mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Wananchi kwa sasa hawasubiri tena kusoma gazeti linalotoka siku ya pili asubuhi au taarifa ya habari katika redio na televisheni, badala yake wengi wao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kupata taarifa za matukio ya moja kwa moja yanatokea katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ni wajibu wetu kutumia mitandao hiyo” alisema Dkt. Abbas.

Mafunzo hayo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti yamehusisha Mikoa 5 ya Morogoro, Tanga, Simiyu, Kilimanjaro na Arusha na halmashauri zake.

Serikali Yaendelea Kuboresha Uwekezaji Katika Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo Ndogo

Katibu Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru akifungua warsha ya siku moja ya tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo Bw. Boniface Michael.

Mwenyekiti Asasi ya Mikono Cultural Heritage Bw. Henry Orauya akieleza jambo kwa Katibu Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru, mara baada ya ufunguzi wa  warsha ya tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo Bw. Boniface Michael.

Katibu Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa warsha ya tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.


Picha na: Frank Mvungi

Na Fatma Salum

Serikali kupitia Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji inaendelea kufanya maboresho ya sekta ya viwanda ili kuendana na kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru wakati akifungua warsha ya siku moja ya tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Meru alieleza kuwa lengo la kufanya tathmini hiyo ni kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye viwanda vidogo na vya kati kwa kuwa kuna mabadiliko mengi yamefanyika tangu sera hiyo ianze kutumika mwaka 2003.

“Viwanda hivyo vinachangia asilimia 27 ya pato la taifa hivyo ni muhimu kupitia upya sera hii na kupata maoni ya wadau kwani hivi sasa kuna mabadiliko mengi ya teknolojia, sheria na taratibu za uwekezaji.” Alisisitiza Dkt. Meru.

Aidha alisema kuwa Serikali itafungua dirisha dogo kwenye Benki ya Uwekezaji (TIB) kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji wa viwanda vidogo na vya kati kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vyao.

Akieleza mipango ya baadae Dkt. Meru alibainisha kuwa Serikali ina mpango wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Viwanda itakayowawezesha wazawa na wawekezaji wengine kupata mitaji yenye riba na masharti nafuu ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.

Dkt. Meru alitoa wito kwa Watanzania kujikita kwenye uwekezaji wa viwanda kwa kuwa ndio njia pekee ya kukuza uchumi kwa haraka na kuongeza ajira, teknolojia, biashara na mitaji.

Tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda imekusudiwa kutoa mwelekeo wa namna bora ya kujikita kwenye uchumi wa viwanda kupitia uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati.